1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Urusi yaulenga mji wa mashariki mwa Ukraine wa Kharkiv

Sylvia Mwehozi
28 Machi 2024

Ukraine inaimarisha hatua za usalama katika mji wake mkuu wa Kyiv baada ya wimbi la mashambulizi ya makombora ya masafa marefu na droni ambayo Urusi imeyafanya usiku wa kuamkia Alhamis.

https://p.dw.com/p/4eEHu
Ukraine Charkiw russische Raketenangriffe
Picha: Vyacheslav Madiyevskyy/REUTERS

Jeshi la Urusi limeendelea kuishambulia Ukraine kwa makombora na ndege za droni, safari hii ni katika mji wa mashariki wa Kharkiv ambako meya wake ameripoti milipuko miwili, ikiwemo mmoja ulioharibu mgahawa. Ripoti za awali zinasema hakuna mtu aliyejeruhiwa. Shambulio hilo la hivi karibuni katika mji wa pili kwa ukubwa wa Ukraine, linatokea baada ya mtu mmoja kuuawa na wengine 19 kujeruhiwa kwenye shambulio jingine la siku ya Jumatano.

Ukraine | Droni
Ndege isiyo na rubaniPicha: Efrem Lukatsky/dpa/AP/picture alliance

Mapema leo, Ukraine ilidai kuzidungua ndege 26 za droni aina ya Shahed za Iran katika miji ya Odesa, Kharkiv, Dnipropetrovsk na Zaporizhzhia, kulingana na mkuu wa jeshi la anga la Ukraine Mykola Oleshchuk aliyechapisha taarifa hizo kupitia Telegram. Milipuko pia imesikika kwenye mji wa Dnipro kusini mwa Ukraine. Soma Putin: Sina mipango ya kushambulia mataifa ya NATO

Wiki iliyopita, Urusi iliulenga mfumo wa nishati wa Ukraine katika mashambulizi ya angani, katika kile Moscow ilichokisema kwamba ni sehemu ya hatua za ulipaji "kisasi" za mashambulizi ya Kyiv kwenye mikoa ya Urusi. Tangu wakati huo, Moscow imezidisha matumizi ya makombora ya masafa marefu, ambayo yana kasi ukilinganisha na makombora ya kawaida na vigumu kuyadungua. Jeshi la Ukraine limesema kuwa litaimarisha ulinzi haswa kwenye mikusanyiko ya umma kutokana na mashambulizi hayo inayohofia yanaweza kufika mbali baada ya kufyatuliwa. 

Baadhi ya Waukraine waamua kutoroka kuliko kupigana na Urusi

Huko Moscow kwenyewe, Ikulu ya Kremlin imesema mazungumzo yanaendelea juu ya uwezekano wa kubadilishana wafungwa, ikijumuisha mwandishi wa habari wa jarida la Wall Street la Marekani Evan Gershkovich, ambaye alikamatwa Urusi takribani mwaka mmoja uliopita kwa makosa ya ujasusi.

Mwandishi huyo raia wa Kimarekani alikamatwa na idara ya usalama ya Urusi ya FSB, na kutuhumiwa kwa ujasusi, ikiwa ni mashitaka ya kwanza dhidi ya mwandishi wa habari wa nchi za Magharibi tangu enzi ya Kisovieti. Gershkovich, waajiri wake na Ikulu ya White House wote wanakanusha vikali tuhuma za ujasusi, wakisema ni mashitaka ya uongo. Urusi yamzuia balozi wa Marekani kumtembelea mwandishi habari aliyekamatwa

Urusi|  Mwandishi wa habari Evan Gershkovich
Mwandishi wa habari wa jarida la Wall Street la Marekani Evan GershkovichPicha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Rais Vladimir Putin alikuwa ameelezea utayari wa kubadilishana mwandishi huyo na kulingana na Kremlin, mazungumzo bado yanaendelea. Mapema wiki hii, mahakama moja mjini Moscow ilitoa uamuzi kwamba Gershkovich, ambaye hapo awali aliwahi kufanya kazi na gazeti la Moscow Times na shirika la AFP, atasalia kizuizini kabla ya kesi yake kusikilizwa mwishoni mwa mwezi Juni.

Washington imeishutumu Moscow kwa kuwakamata raia wa Kimarekani kwa mashtaka yasiyo na msingi ili kuwatumia kama chambo kwenye mazungumzo ya kuachiliwa Warusi waliopatikana na hatia nje ya nchi.