1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miili ya wahanga wa Shakahola yatolewa kwa familia Kenya

Halima Gongo26 Machi 2024

Serikali ya Kenya imeanza rasmi kuzikabidhi familia, miili ya wafu iliyofukuliwa kwenye msitu wa shakahola huko Kilifi pwani ya Kenya. Miili 34 ilitarajiwa kukabidhiwa kwa familia husika Jumanne 26.03.2024.

https://p.dw.com/p/4e93i
Mamlaka nchini Kenya imeanza kuachilia miili ya watu waliofariki katika ibada inayodaiwa kuwahamasisha kufunga hadi kufa kwa njaa
Mamlaka nchini Kenya imeanza kuachilia miili ya watu waliofariki katika ibada inayodaiwa kuwahamasisha kufunga hadi kufa kwa njaaPicha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Zaidi ya familia 30 kutoka maeneo mbalimbali nchini Kenya walikusanyika mapema leo nje ya hospitali ya Malindi katika kaunti ya kilifi kwa ajili ya kupokea miili ya wapendwa wao iliyohifadhiwa katik chumba cha kuhifadhia maiti baada ya kufukuliwa msituni shakahola miezi kadha iliyopita.

''Sina uwezo wa kulizika hiyo miili''

Stephen Mwiti ni miongoni mwa familia za waliokuwa wamefika hapa mapema, Mwiti aliwapoteza watoto sita msituni shakahola na alikuwa na matumaini makubwa ya kuipokea miili hiyo lakini hakufanikiwa. 

''Miili ya watoto wangu nimeambiwa iko hapa. Lakini wale wakaguzi wa serikali wanatakiwa waje hapa. Mimi nimetoka Meru. Hata kama nitapewa hizo miili sijuwi vipi nitayapeleka nyumbani. Sina uwezo wa kulizika hiyo miili'', alisema Mwiti.

Licha ya kuwa serikali ilitangaza kuwa miili 30 kati ya 429 iliyotambuliwa kwa vipimo vya vinasaba (DNA) itatolewa kwa familia, ni familia moja pekee iliyopokea miili minne ya wapendwa wao.

Kero za familia na mashirika ya haki za binadamu

Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya imechukizwa na ucheleweshaji huo
Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya imechukizwa na ucheleweshaji huoPicha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Titus Ngonyo, alimeondokewa na mkewe, mama mkwe wake, mwanawe na mjukuu wake wa miaka mitano. Familia nyengine zilizofika zimerudishwa nyumbani na kupewa tarehe tofauti ya kuja kuichukua miili ya wapendwa wao.

Tume ya kitaifa ya kutetea haki za kibinadamu nchini Kenya KNCHR imelalamika jinsi serikali inavyojivuta kwenye shughuli hiyo ya kukabidhi miili kwa familia za waathiriwa. Mwenyekiti wa tume hiyo Roseline Odede, amelamimikia ukosefu wa vifaa na dawa zinazohitajika kuendeleza kazi hiyo. 

Aidha familia za waathiriwa zimetoa wito kwa serikali kuzingatia ufadhili wa gharama za mazishi. Awamu ya tano ya kufukua miili zaidi katika msitu wa shakahola inatarajiwa kuanza tena baada ya miili iliyopo kukabidhiwa kwa familia.